Mkuu wa mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa amekemea vitendo vya watumishi kuwapatia vitambulisho vya Taifa raia wa nchi za nje kinyemera na kuwa Serikali bado inaendelea kufanya uchunguzi na atakayebainika akifanya kitendo hicho atachukuliwa hatua ya kufukuzwa kazi.
Mwassa ameyasema hayo leo Julai 25 akiwa kambi ya kaboya kikosi 21 KJ wilaya Muleba kwenye ibada maalum ya kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha kwenye vita ya Kagera mwaka 1978/79.
Amesema, “Tunatambua kwamba wapo watu wana dhamana kubwa lakini hawazitumii vizuri, kupitia siku hii nikumbushe kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wote wanaohatarisha Uhuru na usalama wa Taifa letu.
“Hawa ni pamoja na wanaoshiriki kuwaandikisha na kuwapa uraia watu ambao sio Watanzania, tumekwisha baini baadhi na tutaendelea kuchukua hatua stahiki na niseme kwamba hawa wote wanaoandikisha watu wasio Watanzania hawatoamishiwa vituo vingine vya kazi, watafukuzwa kazi,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, ameongeza kuwa “tuna kila sababu na wajibu wa kulinda mipaka ya Kagera tumepakana na nchi nyingi na wenzetu wamelala hapa walipigania uhuru hatutoruhusu na hatutokubali kuona Mtanzania mwingine anachezea amani yetu na anahatarisha usalama wa Taifa letu”.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa vita ya Kagera hufanyika kila mwaka ifikapo Julai 25 ambapo hii leo kimkoa imefanyika wilaya ya Muleba kwenye kambi ya Kaboya kikosi 21 KJ ambapo zaidi ya mashujaa 600 walizikwa katika kambi hiyo.