Mkutano wa siku tatu wa Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika, umeanza hii leo Novemba Mosi, 2022 Visiwani Zanzibar, ukitaraji kuzungumzia na kushughulikia changamoto zinazowakabili nchi wanachama kupitia Mabunge.
Mkutano huo ambao umewashirikisha wajumbe 150 kutoka nchi 18, umefunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, ambaye amewataka washiriki kujadili mambo mbalimbali yanayoweza kuleta maendeleo.
Amesema, “Wanasheria wa mabunge husika shirikini katika kutunga sheria na sera, ambazo baadae zitajadiliwa na kupitishwa na wabunge, Sheria na sera hizi ni muhimu katika kufikia malengo ya kila nchi.”
Rais Mwinyi ameongeza kuwa, sera na sheria nzuri ambazo zina nafasi kubwa ya kuharakisha maendeleo yaliyo na umuhimu katika kubadilisha maisha ya watu kiuchumi na kijamii, huku Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zubeir Ali Maulid alisema wanasheria ambao wanafanya kazi katika mabunge watapata uzoefu mkubwa kupitia mkutano huu.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika anayameliza muda wake, Mussa Kombo amesema tangu kuundwa kwa chama harakati za nchi wanachama za kuwa na sera na sheria kupitia mabunge zimesaidia kuleta mageuzi katika nyanja mbalimbali, ambapo pia akawaomba wanachama kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Chama cha Wanasheria wa Mabunge ya Afrika, kiliasisiwa mwaka 2011 jijini Nairobi nchinu Kenya, kikiwa na lengo la kujenga uhusiano wa karibu na kubadilishana taarifa, uzoefu na ujuzi baina ya wanasheria wanaohudumia mabunge ya Afrika.