Wapinzani wa vyama vya Siasa nchini, wametakiwa kuacha kupinga kila kitu kinachofanywa na Serikali kwani suala hilo linarudisha nyuma nguvu kazi ya Taifa na waelewe kuwa Chama cha Mapinduzi – CCM hakina ubaguzi katika suala la utekelezaji wa maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media hivi karibuni na kusema, ukiwa mpinzani haimaanishi upinge kila jambo hata kama ni jema kwani kufanya hivyo hawaikomoi Serikali.
“Vyama vya upinzani vinatakiwa kujadili hoja na sio tu kujadili namna ya kumtoa kiongozi aliyepo madarakani na kizuri wakipokee, Serikali haibagui na ndiyo dhana ya CCM, kuna majimbo mengine yameendelea vizuri licha ya kuwa yanaongozwa na upinzani,” Amesema Dkt Kimei.
Akizungumzia suala la ukimya wake katika vyombo vya Habari, Dkt. Kimei amesema “unapoelewa mambo halafu ukaona watu wanavuruga unajisemea acha nikae kimya, sitaki kujenga uadui na watu, unaacha watu waseme na kama ni ushauri basi unautoa kwa anayehusika na si kuongea kwenye media nimejifunza kutotoa siri.”