Wanaume wametakiwa kujitokeza kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi ili kuzijua afya zao na si kutegemea matokeo ya wake zao.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa wakati akizungumza na washiriki na wadau mbalimbali kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, mara baada ya kushiriki matembezi hayo kwa Km. 5 ambayo yameratibiwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT).
Majaliwa amewaomba Viongozi wa Dini kuwa mastari wa mbele kuwasisitiza watu kujua hali zao hasa wanaume ambao wamekuwa nyuma katika hilo.
“Wanaume jitokezeni mkapime, msitegemee matokeo ya wake zenu. Mimi ndiye Balozi wa kuhamasisha wanaume kupima virusi vya UKIMWI, kwa hiyo msiniaibishe. Kuanzia leo, nendeni kwenye vituo vyetu mkapime VVU.”
“UKIMWI bado upo, ninawaomba suala hili lipewe kipaumbele wakati wa mahubiri, hotuba na mihadhara. Endeleeni kuwakumbusha waumini kuhusu umuhimu wa kubadili tabia hususan zile zinazochangia maambukizi.” amesema Majaliwa
“Jana ilikuwa ni maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani. Kwenye tathmini yetu, malengo ya 95-95-95 yamefanikiwa kwa maana ya 95 ya kwanza imeongezeka kwa sababu watu wengi wamejitokeza kupima. Hii inahamasisha upimaji na watu wanaojitokeza ni wengi lakini wanaopima sana ni wanawake. Wanaume hamuendi kupima.”
Aidha, amewataka viongozi hao wawaangalie zaidi vijana kwani ni kundi lililo kwenye hatari zaidi. “Kwa kuwa kundi la vijana liko katika hatari zaidi ya kupata maambukizi, ninawasihi sana imarisheni huduma za unasihi na malezi. Ninayo imani kuwa, kwa nafasi zenu ndani ya jamii, vijana watawasikia, watawatii na kubadilika.”