Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Omari Kumbilamoto amezindua Taasisi ya Mtandao wa Wanawake kwenye Sekta ya Nishati (TAWOE) na programu mpya zilizopo katika taasisi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Kumbilamoto amewataka wanawake waliopo katika sekta za nishati kujiamini na kufanya kazi kwa weledi huku wakitakiwa kutokukata tamaa ili kuweza kukuza sekta ya nishati hapa nchini.
Aidha ameahidi kuwa mstari wa mbele kuisaidia taasisi hiyo ambayo imeonesha nia ya dhati kuinua wanawake katika sekta ya nishati na kuweza kutatua changamoto mbalimbali.
“Katika kuunga mkono TAWOE ameahidi kuisaidia taasisi hiyo katika kutatua changamoto zinazoikabili huku akiweka wazi kuwa tayari jiji limekwisha tenga asilimia Nne ya mapato yake kwenda kwa kina mama”. Amesema Kumbilamoto.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya TAWOE Mhandisi Gwaliwa Mashaka, amesema kupitia uzinduzi huo utasaidia kuwawezesha wanafunzi hasa wakike katika kuonyesha kile wanachokifanya.
Nae mmoja wa washiriki ambaye ni mshauri muelekezaji masuala ya umeme kutoka katika kampuni ya Gein Energy Product Farm Dkt.Juliana Palangyo amesema wanawake wengi wapo katika sekta za nishati na wanajitahidi kwa weledi mkubwa huku changamoto kubwa ikionekana ni kutokukubalika.