Zaidi ya Wanawake Vijana 2,000 ambao hapo awali walikatisha masomo, wamejiunga na program ya Elimu Haina Mwisho (EHM), inayolenga kuwawezesha kufikia malengo yao kielimu kwa kuwapa fursa ya kurejea shuleni.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na Shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO), iliyotolewa hii leo Agosti 30, 2022 jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imesema, programu hiyo inalenga kuwawezesha wanawake vijana kufikia malengo yao kielimu ya masomo ya Sekondari kupitia mfumo usio rasmi, masomo ya ufundi, ujasiriamali na stadi za maisha.
Rais Samia: ‘Polisi ikifanya vibaya tatizo limeanzia juu’
Aidha, katika kuendeleza maarifa kwa wanawake vijana waliokatisha masomo, Shirika hilo limekabidhi msaada wa Vitabu 3,195 vya masomo ya Sekondari, miongozo na vitini vya kufundishia fani mbalimbali za ufundi kwa washiriki wa programu hiyo ya EHM.
Vitabu vingine ni vya masomo bobezi katika programu ya mafunzo ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto au ualimu wa chekechea ambavyo vimekabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya ufundi (TVET) katika Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia (WyEST), Dkt. Noel Mbonde.
Msaada huo wa vitabu una thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 70 ambavyo vingine ni vya miongozo ya ufundishaji wa fani mbalimbali za ufundi katika vyuo 54 vya maendeleo ya wananchi katika fani za Kilimo, Uashi, Ufugaji, Upishi, Ufundi magari, Ubunifu wa mavazi, na umeme wa majumbani.
Kashfa Jeshi la Polisi kwa kuuwa watu 14
Aidha taarifa hiyo imeitaja mikoa ambayo inatekeleza mpango wa EHM kwa wanawake vijana kuwa ni Arnatutouglu (Dar es Salaam), Bariadi (Simiyu), Buhangija (Shinyanga), Chala (Rukwa), Chilala (Lindi), Gera (Kagera), Kilosa (Morogoro) na Kisangwa (Bunda).
Mikoa mingine ni Msingi (Singida), Musoma (Mara), Nandembo (Ruvuma), Tarime (Mara) na Ulembwe (Njombe), na msaada huo wa Vitabu ukiunga mkono jitihada za Serikali za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya maendeleo ya Wananchi (FDCs).