Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi, Asia Matauka amewataka wakina mama kutambua kwamba wana nguvu kubwa katika kuziombea familia zao, hivyo wasikate tamaa kwani Taifa linawategemea.
Asia ameyasema hayo wakati akiongea na Waumini wa Kanisa la Power Of Faith International – PIC, lililopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, katika sikukuu ya Wanawake wa Kanisa hilo.
Amesema, “Wanawake ni Jeshi kubwa katika maombi hivyo mnapaswa kumlilia sana Mungu kwa kuomba ili kuhakikisha familia zenu zinakombolewa na kuacha matendo mabaya yenye kuleta taswira mbaya kwa jamii.”
Asia pia amewasisitiza Wanawake hao kuendelee kuwa karibu na familia zao kwa kuwafundisha mambo muhimu yenye kuwapa maarifa, kutenda matendo mema yenye maadili na kuwajengea uwezo wa kujitegemea katika maisha yao ya kila siku.
Katika hatua nyingine, SP Asia amewakumbusha Wanawake kuendelea kujikita katika shughuli za uzalishaji mali na kuachana na mikopo ya kausha damu isiyokuwa na tija kwa maendeleo yao.