Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) makao makuu kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya mashtaka imewafikisha mahakamani watuhumiwa watano leo Agosti 31, kwa tuhuma za rushwa, uhujumu uchumi na ukwepaji kodi wa kiasi cha shilingi milioni 153.5
Watuhumiwa waliofikishwa mahakamani ni Ajuaye Kheri Msese aliyekuwa Meneja wa bandari Kigoma, Herman Ndiboto Shimbe aliyekuwa Afisa uhasibu TPA Kigoma, Jesse Godwin Mpenzile Aliyekuwa mhandisi mkazi kigoma TPA, Lusubilo Anosisye Mwakyusa aliyekuwa Afisa rasilimali watu TPA Kigoma na Rodrick Ndeonakia Uiso Mkurugenzi Kampuni ya M/S Saxon Buildings Contractors Limited.
Kati ya watuhumiwa hao, wanne ni watumishi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania mkoa wa Kigoma ambao kwa sasa wameshafukuzwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani, TAKUKURU inaendelea kufanya uchunguzi kwa lengo la kubaini kiasi kingine cha fedha kilichohujumiwa ikiwa ni pamoja na kumtafuta Madaraka Robert Madaraka aliyekuwa mhasibu bandari ya Kigoma ili aweze kuunganishwa katika shauri hili.