Polisi nchini Marekani imethibitisha kuwa mwanamke mmoja aliyepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea baada ya wafuasi wa Trump kuvamia bunge, amefariki dunia kutokana na majeraha aliyopata.
Aidha, mtu mwingine amepigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea ndani ya bunge la Marekani, huku mwanahabari Lindsay Watts, kutoka shirika moja la kihabari nchini humo akiandika ujumbe kwenye Twitter kuwa wahudumu wa afya wa Washington DC walisema juhudi za kumuokoa mwanamke mmoja aliye kwenye hali mahututi zinaendelea baada ya kupigwa risasi kifuani.
Wafuasi wa Donald Trump wenye hasira wamevuka mipaka ya usalama iliyowekwa na kusimama kandokando ya bunge huko Washington, wakati wabunge wanakutana kumuidhinisha rais mteule Joe Biden kama mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.
Wafuasi hao waliandamana wakiimba, “Tunamtaka Trump” huku mmoja wao akipigwa picha akiwa ameketi kwenye kiti cha rais wa bunge la Seneti.
Maafisa polisi wa Washington DC wamesema hadi kufikia sasa watu 13 na silaha tano zimenaswa na polisi wakati ghasia zinaendelea bungeni, huku Mkuu wa polisi Robert Contee amewaambia wanahabari kuwa waliokamatwa sio wakazi wa eneo la DC.
Baada ya uvamizi huo uliochukua saa kadhaa, afisa anayesimamia mipangilio ya Bungeni alitangaza kuwa sasa jengo hilo limenusuriwa na vikosi vya usalama na wakati mmoja Trump alilazimika kurekodi ujumbe kwenye video na kuutuma katika mtandao wa Twitter akitoa wito kwa wafuasi wake kuondoka katika majengo ya bunge lakini naye akawa anaendelea madai kuwa Democrats waliiba kura.
“Najua machungu yenu, najua mumevunjika moyo, lakini lazima sasa mrejee nyumbani, lazima tuwe na amani … hatutaki yeyote ajeruhiwe, ” amesema Trump.
Licha ya ujumbe huo wa Trump kwa waandamanaji wanaomtaka asalie madarakani, kumekuwapo na ishara kidogo zinazoonesha kwamba waandamanaji hao wanatii wito wa Trump kuwataka warejee nyumbani licha ya kwamba mji huo wote unatekeleza hatua ya kutotoka nje kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi kumi na mbili asubuhi.
Kikao cha pamoja cha Bunge kuidhinisha ushindi wa Biden kimeahirishwa na Bunge limelazimika kwenda mapumzikoni.