Watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, wamesimamamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa Shilingi milioni 300 za ujenzi wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Nsimbo, na kutoa siku 30 za kukagua miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo, ikiwemo vituo vya afya, shule na vituo vya tozo.
Agizo la kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, lililotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko kufuatia udanganyifu kuhusu matumizi ya fedha hizo, baada ya kufanya ziara ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo, ambapo amebaini matumizi mabaya ya fedha za Serikali.
Waliosimamishwa kazi ni Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mkuu wa Idara ya Afya, Ofisa Mipango pamoja na mkaguzi wa ndani, ambapo pia amemuelekeza mkaguzi wa ndani wa Mkoa, pamoja wataalam wengine waliopo chini ya Katibu Tawala wa Mkoa, kukagua namna pesa hizo zilivyotumika.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameiagiza TAKUKURU Mkoa wa Katavi kukagua kwa undani mradi mzima wa hospitali ya Wilaya Nsimbo, ili kubaini ubadhirifu uliofanyika wa matumizi ya fedha, ubora wa mradi, ununuzi wa vifaa na thamani zake na kuchukua hatua za kisheria endapo watabaini kuwepo na hitilafu.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yusuf alimwambia Mkuu wa Mkoa kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, baada ya kufuatilia matumizi ya Shilingi milioni 300, waliambiwa mililioni 210 zimetumika katika matumizi nje ya lengo lililokusudiwa, hivyo kumuagiza Mkurugenzi kufuatilia matumizi ya fedha hizo.