Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Ludewa mjini wametishia kuacha kunywa Pombe za kienyeji, hadi pale Serikali itakapowajengea Kilabu cha Pombe, na kudai kuwa inapoteza mapato katika eneo hilo.
Wananchi hao, wametoa tishio hilo mbele ya Mbunge wao Joseph Kamonga, na kusema Serikali inapoteza mapato kutokana na kukosekana kwa Vilabu vya pombe za kienyeji katika maeneo yao.
Wamesema, si watu wote ambao wana uwezo wa kunywa Pombe za kisasa na kwamba wanashindwa kupata huduma katika vilabu vya watu ambao wanatoa huduma bila kutambuliki na mamlaka za Serikali.
Mbele ya Mbunge huyo wa jimbo la Ludewa, mmoja wa Wananchi hao alisema wanafikiria kuanzisha mgomo wa kunywa pombe hizo hadi pale Serikali itakapotatua tatizo lao la kukosa kilabu cha pombe za kienyeji.
Ansila Kayombo, mmoja kati ya waliosimama na kutoa maelezo hayo amesema, “Wenzetu wote vijijini huku wana kilabu cha kijiji, sisi miaka yote hatupati tunaomba sana kusaidiwa ama sivyo tutagoma.”
Akijibu hoja hiyo, Diwani wa kata ya Ludewa, Monica Mchilo amewahakikishia wananchi kuwa uongozi wa kijiji utaangalia uwezekano wa kuanza ujenzi wa hitaji lao, huku Mbunge wa jimbo hilo akiwaomba viongozi kutatua kero hiyo.