Wapiganaji kutoka jimbo lililokumbwa na mzozo la Tigray, Ethiopia wameonya kwamba wanajeshi wao watatafuta mbinu za kuharibu uwezo wa vikosi vya Ethiopia na Eritrea, licha ya serikali ya Ethiopia kutangaza sitisho la mapigano la upande mmoja katika jimbo hilo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Voice of Amerika (VOA) Serikali ya Ethiopia ilitangaza sitisho la mapigano kupitia vyombo vya habari vya nchi hiyo na kusema kwamba litaanza kutekelezwa mara moja.
Taarifa ya sitisho hilo la mapigano imejiri baada ya miezi minane ya mzozo huko Tigray, wanajeshi wa chama tawala cha zamani katika jimbo la Tigray waliingia katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle, na kulakiwa kwa shangwe na wakazi wa mji huo.
Msemaji wa vikosi vya Tigray Jumanne ameonya katika mahojiano na shirika la habari la Reuters kwamba wanajeshi wa Tigray wataingia katika nchi jirani ya Eritrea na katika jimbo la Ethiopia la Amhara, kuvisaka vikosi adui iwapo itahitajika.