Rais wa zamani wa Brazil, Luis Inacio Lula da Silva ameshinda duru ya pili ya uchaguzi baada ya kumuangusha mpinzani wake, Jair Bolsonaro na kutoa mwito wa amani na umoja baada ya uchaguzi huo huku akiwalaumu wapinzani wake kutaka kumzika akiwa hai.
Mwanasiasa huyo wa mrengo wa kushoto, anayetambulika zaidi kwa jina la Lula amembwaga Bolsonaro kwa ushindi mwembamba wa asilimia 50.9 dhidi ya asilimia 49.17 za mpinzani wake.
Akiongea mara baada ya ushindi huo Lula amesema, “Ninajiona kama raia wa Brazil ambaye anakabiliwa na mzigo wa kuzijenga upya siasa za Brazil Kwa sababu wapinzani wangu walijaribu kunizika nikiwa mzima na leo niko hapa, kuitawala nchi na kuitoa kwenye hali ngumu sana.
Kupitia hotuba yake, aliyoitoa jijini Sao Paulo Lula amebainisha kuwa, ushindi huo ni wa watu wa Brazil na si wake pake yake ama chama chake cha Wafanyakazi, na pia ni ushindi wa vuguvugu la demokrasia iliyoko juu ya vyama vya siasa na maslahi binafsi ya kiitikadi.
Ameongeza kuwa, “Lakini nina imani kwamba kwa msaada wa watu tutapata suluhu ya kuliondoa taifa hapa lilipo na kurejea kwenye demokrasia na amani ili tuweze kuwasaidia wazazi wetu, familia na kuujenga ulimwengu ambao watu wa Brazil wanautaka. “
Hata hivyo, ametoa wito wa amani na umoja huku akiapa kupambana na njaa na kuulinda msitu wa mvua wa Amazon katika utawala wake, bila kuweka kando mikakati ya kurejesha sera muhimu za kiuchumi na kuboresha hali ya maisha.