Wapinzani nchini Venezuela wameivunja Serikali ya mpito iliyokuwa inaongozwa na Juan Guaido aliyekuwa anatambuliwa kimataifa, kutokana kushindwa kuuangusha utawala wa kiongozi wa mrengo wa shoto Nicolas Maduro.
Tukio hilo, linafuatia kupigwa kwa kura kwenye kikao cha mtandaoni cha bunge linalodhibitiwa na wapinzani, ambalo lilianzishwa Kama baraza mwaka 2015 ambalo sasa limebakia kuwa la ishara baada ya mahala pake kuchukuliwa na bunge linalomtii Maduro.
Aidha, katika majumuisho kura 72 ziliunga mkono kuvunjwa kwa serikali hiyo ya mpito na 29 zilipinga huku Wajumbe wanane wakiwa hawakupiga kura na Serikali hiyo ya mpito ilitambuliwa na nchi zipatazo 50, ikiwa ni pamoja na Marekani.
Licha ya wapinzani kudhibiti sehemu ya mali za Venezuela zilizopo nchi za nje, ukosefu wa mkakati wa kumwondoa Maduro madarakani ulisababisha kuanguka kwa umaarufu wa Guaido na pia umepungua kimataifa baada ya Marekani kuchukua msimamo mnyumbuko.