Vyama vya kisiasa nchini Afrika Kusini, vimekubaliana kuunda Muungano wa kukiondoa Chama tawala cha ANC madarakani, iwapo hakitapata wingi wa viti kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao wa 2024.
Taarifa toka nchini humo, zinasema miongoni mwa vyama hivyo ni pamoja na Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance na vingine sita, vikikubaliana kuwa na muundo wa Multi-Party Charter for South Africa.
Makubaliano hayo yamefanyika ikiwa ni siku mbili baada ya mkutano wa Kempton Park, Johannesburg huku ANC ambacho ni chama cha Hayati Nelson Mandela, kikitarajia kufikisha miaka 30 tangu kupata kwa uhuru wa taifa hilo.
ANC, kiliongoza vuguvugu dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kikachukua usukani wa Afrika Kusini kufuatia uchaguzi mkuu wa 1994 na Nelson Mandela kuchaguliwa kuwa rais wa kwanza mzawa.