Boniface Gideon- Tanga.
Mfuko wa Utamaduni na Sanaa nchini, umetoa mafunzo kwa wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Tanga yanayolenga kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuchukua mkopo na kurejesha kwa wakati kufuatia Serikali kutoa Bilioni 20 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mtendaji mkuu wa mfuko huo, Nyakaho Mahemba amewaambia wasanii hao kuwa Serikali imeweka bajeti hiyo kwa lengo la kuwawezesha wasanii kupata fursa ya kuchukua mikopo mikubwa ambayo itawasaidia kuinuka kiuchumi.
‘’Rais Samia anawapenda sana wasanii na ndio mana ametoa fedha hizi, mkopo huu una riba ya asilimia 9 tu na hakuna mkopo ulio na riba nafuu kushinda huu na uzuri wake mnaweza kukopa kama kikundi au mtu mmoja mmoja, lakini pia hauna masharti mengi ikiwamo dhamana ‘’ alisisitiza Mahemba.
Kwaupande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Sebastian Masanja aliwataka wasanii hao kutumia fursa hiyo ya mkopo na kuwakumbusha nidhamu ya matumizi ya fedha hizo.
Alisema, ‘’itumieni fursa hii kwa kuhakikisha mnachukua mikopo na muwe wabunifu wa miradi ili muinuke kiuchumi lakini msisahau nidhamu ya matumizi ya pesa hizi mkumbuke huu ni mkopo sio pesa za msaada unatakiwa uzirudishe tena kwa wakati,’’ alisisitiza Masanja.