Meneja wa Manchester United, Eric ten Hag amewaambia mabosi wa timu hiyo kwa gharama yoyote ile wamsajili mshambuliaji halisi wa kati ambaye atakuja kulipa makali eneo hilo.
Meneja huyo kutoka Uholanzi ametoa kauli hiyo baada ya kuona eneo hilo halina makali pale ambapo Marcus Rashford ambaye ndiye kinara wa mabao klabuni hapo anapokesekana.
Mabosi wa Man United kwa sasa wamekuwa wakifanya jitihada za kuinasa saini ya straika wa Tottenham, Harry Kane ambaye thamani yake inatajwa kuwa Euro milioni 100.
Ten Hag amesema: “”Kila mtu anajua hilo na wala siyo siri kuwa msimu wote huu tulikuwa na uhaba wa mastraika namba tisa.
“Tulilazimika kumuondoa [Cristiano] Ronaldo, na wakati huo Anthony Martial hakuwa anapatikana pia Jadon Sancho hakuwa anapatikana na nikawa na wachezaji wachache wa eneo hilo.”
“Tuna wachezaji ambao wanaweza kucheza eneo hilo lakini kiukweli tunahitaji mshambuliaji ambaye atakuwa na mchango na mwenye kiwango cha juu,” alimalizia Meneja huyo. Kando ya Kane United pia wanahusishwa na washambuliaji Victor Osimben wa Napoli, Jonathan David (Lille), Rasmus Hojland (Atalanta), Tammy Abraham na Dusan Vlahovic wa Juventus.