Aliyewahi kuchukua fomu ya kugombea urais uchaguzi mkuu 2015, na mbunge wa Bunda katika serikali ya awamu ya nne, Stephen Wasira, amesema kuwa si jinai kuikosoa Serikali bali kuitukana ndiyo kosa kisheria.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini amewasihi wananchi kuendelea kuikosoa Serikali na si kuitukana.
Amesema kuna tofauti kubwa kati ya kutukana na kukosoa.
‘Mimi naweza nikasema na bado nisitukane, mfano Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma huwa nasoma maandiko yake anaonekana akijenga hoja kabisa inayohitaji kujibiwa na sijawahi kusikia akikamatwa’’ amehoji Wasira.
Aidha ameeleza kuwa wapo wanasiasa ambao mazungumzo yao mara nyingi huwa ni ya kuitusi Serikali na ndio maana Serikali pia huwashughulikia watu wa namna hiyo na kuwachukulia sheria.
Pia ameliomba jeshi la polisi kufanya kazi kwa uangalifu na kulisisitizia kuwa watu wasiokuwa na hatia wasikamatwe.