Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameagiza wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Daraja la J.P. Magufuli (kigongo – busisi) lenye urefu wa kilometa 3.2 kuhakikisha wanaongeza ushiriki wa wahandisi wazawa katika utekelezaji wake.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unaogharimu zaidi ya kiasi cha bilioni 716 ambazo zote ni fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki ya watanzania kujifunza na kusimamia rasilimali hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Prof. Mbarawa ameyasema hayo jijini Mwanza, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Sengerema mara baada ya kumaliza kukagua daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 34.
“Ujenzi wa Daraja hili unaandika historia kwa nchi yetu kwa ukubwa na viwango vya kisasa hivyo liwe shule tosha kwa wahandisi wa ndani ili kuwawezesha kuweza kujenga madaraja kama haya nchini”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo kwa wakati na kwa hivyo wakazi wa Mwanza na mikoa jirani wasipate hofu juu ya mradi huo kwani utamalizika kwa wakati na viwango vilivyowekwa.
“Katika kipindi chote mkandarasi yuko hapa analipwa fedha kulingana na kazi zinazoendelea na mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari, 2024”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa daraja hilo litakapokamilika litakuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati na litakuwa ni la sita (6) katika Bara la Afrika kwa takwimu za sasa.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa Daraja hilo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Boniface Mkumbo, amemueleza Waziri huyo kuwa mradi umetoa ajira 720 ambapo kati ya hizo ajira 663 ni za watanzania na 57 ni za wageni.
Mhandisi Mkumbo ameeleza kazi kubwa zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa daraja wezeshi, nguzo ya kwanza na ya pili kwa upande wa Kigongo umekamilika, ujenzi wa matabaka ya barabara za maingilio kwa pande zote mbili, ujenzi wa karakana ya kukunjia vyuma na ujenzi wa mitambo ya kuchanganya zege na kusaga kokoto zimekamilika.