Katika kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti wa ugonjwa wa Kimeta na Kichaa cha Mbwa nchini wataalamu wa Afya ambao ni wataalamu wa sekta za Afya ya Binadamu, Afya ya Wanyama wafugwao na Wanyamapori pamoja na sekta ya Mazingira, wameitaka serikali kuanzisha wiki ya chanjo kwa mifugo nchini.
Wameyasema hayo jijini Arusha wakati wa Mkutano wa Ujirani wa kujiandaa kujikinga na udhibiti wa magonjwa, uliowakutanisha wataalamu hao kutoka katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma, ambapo wamebainisha kuwa wameamua kutoka na azimio hilo.
Mkurugenzi Msaidizi, Kitengo cha Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Janneth Mghamba,amesema kuwa Wizara imekuwa ikipokea taarifa za ugonjwa wa Kimeta mara kadhaa katika baadhi ya Wilaya za Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
“Kinga ni bora kuliko matibabu, hivyo ili kudhibiti haya magonjwa yanayotoka kwa wanyama hatuna budi kujikita katika chanjo ya wanyama hao ili kupunguza maambukizi ya wanyama hao kwa binadamu,”amesema Mghamba
Hata hivyo, Mghamba ameongeza kuwa , katika kuhakikisha kunakuwepo na mikakati ya udhibiti wa ugonjwa huo imewakutanisha wataalamu wa afya wa mikoa husika kwa kutumia dhana ya afya moja ili waweze kujadili kwa pamoja na kuwa na mipango ya udhibiti ya pamoja kwani magonjwa hayana mipaka, Aidha hatua hiyo ya kuwa na mikakati ya pamoja itaweza kupunguza gharama za udhibiti wa magonjwa.