Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kujibidiisha katika utendaji wao na kuhakikisha wanakuwa na takwimu sahihi za matukio ya ukatili badala ya kutegemea taarifa za Jeshi la Polisi ambazo utolewa na Mkuu wa Jeshi hilo baada ya mwaka mzima.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wataalamu wa maendeleo ya Jamii linaloendelea kwa siku mbili.
Amesema baadhi ya wataalamu wa afya wamekuwa wakimpatia taarifa zenye takwimu kwa wakati na kuwataka kuiga mfano huo na kuwa wanawasiliano ya karibu na vituo vya Polisi Mikoani ili waweze kupata taarifa za wahanga wa ukatili katika maeneo yao kazi.
“Wataalam wa maendeleo ya jamii wamekuwa hawanipi taarifa hata nikiwa katika ziara kwenye maeneo yao na hata ninapowauliza wanakuta hawana taarifa yoyote ile kuhusina na masuala yanayohusiana na maendeleo ya jamii hivyo ni vyema kujibidiisha ili taarifa ziwepo kwa wakati,’’ ameongeza Ummy.
Kufuatia hali hiyo Waziri Ummy amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike kuweka mfumo mzuri wa kukusanya takwimu za maendeleo ya jamii ili kuwezesha kupatikana kwa takwimu ndani ya muda muafaka na kwa haraka.
Sambamba na kutoa hamasa hiyo kwa wataalam hao pia amewataka kuhamasisha jamii ili iweze kutumia teknolojia ya habari kwa ajili ya kujiletea maendeleo na kwani taarifa zinazopatikana zitasaidia jamii kupata masoko ya bidhaa zao ikiwemo elimu juu ya kilimo bora.
‘’Nipate taarifa sahihi na kwa wakati kila nikija katika Mkoa au Halmashauri, ukiongea na takwimu ni rahisi kupata rasilimali fedha na misaada mingine itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo kama za vikundi vya wajasiliamali ambao wamepokea mikopo ya Halmashauri hii ni njia rahisi ya kutatua matatizo,’’ amefafanua Waziri Ummy.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ameitaka jamii kuacha kutumia muda mwingi kufuatilia mitandao ya kijamii na badala yake wahamasishwe kufanya mambo yenye tija kwa maendeleo yao na kupunguza starehe kwa kutumia fedha nyingi kwenye mambo yasiyo na msingi.
“Jamii ya watanzania inapenda starehe sana na watu wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya kusherekea harusi, siku ya kuzaliwa wanatakiwa kujiuliza vipI kuhusu ada kwa ajili ya mwanafunzi na kujiwekea akiba ya baadae maishani,” ameongeza Ummy.
Hata hivyo amewataka wataalam hao kufikiria kuwekeza katika miradi ambayo ina mashiko na kukemea tabia ya wafadhili kuweka mkazo katika masuala ya warsha na Semina ambazo hazitoi matokeo ya moja kwa moja katika jamii.
Awali akizungumza kwa Niaba ya katibu Mkuu Maendeleo ya jamii Mkurugenzi wa maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema jukumu kubwa la wataalam hao ni kuiandaa jamii katika ushiriki wa shughuli za maendeleo ya nchi ili iweze kusonga mbele katika mambo mbalimbali.
wa Maendeleo ya Jamii Sunday Wambura amesema mkutano huo mkuu wa mwaka umeambatana na uzinduzi wa chama kitakachowasaidia kupeana mbinu mbalimbali za kuhakikisha maafisa wanaisaidia jamii kimaendeleo.
Wataalamu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii wanakutana Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa mwaka kwa lengo la kukumbushana majukumu yao ikiwemo kupata maarifa mapya na kuandaa mada mbalimbali zitakazotolewa katika mkutano huo.