Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wakati umefika kwa wataalamu wa mifugo kujengewa uwezo ili kutoa huduma maeneo ya vijijini, kulinda usalama wa mifugo, na mazao yatokanayo na mifugo.
Waziri Ulega ameyabainisha hayo hii leo Novemba 15, 2022 jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), kwa wataalamu wa mifugo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na baadhi kutoka nchi zingine duniani.
Amesema, lengo la kuwakutanisha wataalamu hao ni kuwajengea uelewa wa pamoja na kupanga mikakati namna wanavyoweza kusaidiana na wataalamu wasaidizi kukuza sekta ya mifugo katika nchi zilizopo kwenye jumuiya hizo na kwamba idadi ya madaktari na wataalamu wa mifugo waliopo nchini haitoshelezi nchini.
“Wafugaji wengi wapo vijijini kwa idadi ya madaktari au wataalamu wa mifugo tulionao haitoshelezi kusema wataenea kote, tunao kama 5,600 kote nchini ukilinganisha na ukubwa wa sekta ni wakati wa kuweka mikakati namna ambavyo tunaweza kuwasaidia kufika hadi vijijini,” amebainisha Naibu Waziri.
Kwa upande wake, msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania (VCT), Dkt. Amani Kilemile amesema majukumu waliyonayo ni kuhakikisha huduma za matibabu ya mifugo zina kuwa bora kwa kufuata sheria zilizoanzisha baraza hilo kwa kusimamia pia ubora wa elimu kwa wataalamu wa mifugo kuanzia ngazi ya cheti.
Kongamano hilo, linalowahusisha wataalamu wa mifugo kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na baadhi kutoka nchi zingine duniani, lililoandaliwa na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH), linalenga kubadilishana uzoefu wataalamu wa mifugo katika njia ya utendaji kazi na kuweka mikakati ya namna ya kuboresha sekta ya mifugo.