Serikali ya wilaya ya Sengerema imeanza kuifanyia kazi sheria ndogo ya kuwacharaza bakora 12 na faini ya shilingi 10,000 wanaume watakaokutwa wamesimama na wanafunzi wa kike ikiwa ni hatua za kupunguza mimba shuleni.
Kata ya Nyehunge imekuwa ya kwanza kutilia mkazo sheria hiyo kupitia kikao chake maalum, ambapo mbali na hatua hiyo imewakamata wanafunzi watano waliopata ujauzito mwaka jana.
Sheria hiyo imepitishwa rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao cha maendeleo kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kata.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Mabula Enock amesema kuwa wamechukua hatua hiyo kutokana na kuongozeka kwa idadi ya wanafunzi wanaopata ujauzito na kukatisha masomo yao, na kwamba wanaungana na kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya hiyo, Emannuel Kipole alilolitoa mwaka jana.
“Tunaungana na agiza la mkuu wetu wa Wilaya, Emannuel Kipole aliyeagiza kuwachapa viboko 12 na faini ya shilingi 10,000 wanaume watakaokutwa wamesimama na wanafunzi wa kike,” Enock anakaririwa na gazeti la Mwananchi.
Kauli hiyo iliungwa mkono na diwani wa kata hiyo, Charles Mbogo ambaye alitaka kuongezwa kwa adhabu hiyo kwani kuongezeka kwa wanafunzi wanaopata mimba na kulazimika kukatisha masomo hakuvumiliki.
- Wingi wa wanafunzi kidato cha kwanza kupelekea kuanzishwa shule mpya.
- 13 wauawa kwa risasi wakitafuta kuni
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Afisa Elimu wa Sekondari wa Buchosa, Benjamini Separato wanafunzi wa kike 18 walipata ujauzito katika mwaka wa masomo 2016/2017, kati ya jumla ya wanafunzi 1,136 wa shule 20 zilizopo katika wilaya hiyo.