Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameamuru kutiwa mbaroni matapeli watano maarufu wa kuuza na kunyanganya ardhi za watu Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo katika mkutano wa kusikiliza kero za migogoro ya ardhi ya wakazi wa Mkoa wa Pwani na kuzitolea ufumbuzi eneo la Mapinga Wilaya ya Bagamoyo mkoani wa Pwani, ambapo wakazi wa eneo hilo walitoa ushuhuda wa kutapeliwa ardhi zao.
Aidha Watuhumiwa hao ni Omari Shabani ambaye ni Katibu Muenezi wa kata ya Mapinga, Ramadhani Rashidi aliyekuwa katibu wa kitongoji cha Kiembeni, Marwa Muhoni, William Urio na Mwanahamis Habibu.
“Matapeli wengi wa ardhi hapa mkoa wa Pwani hasa Bagamoyo ni viongozi, viongozi wa mitaa na kata wanafanya utapeli, viongozi hata wa chama nimekuta kule viongozi wa mashina wanasaini nyaraka za mauziano ya ardhi,” Amesema Waziri Lukuvi.
Naye Diwani wa kata ya Mapinga Chandika Dismas pamoja na baadhi ya viongozi walikiri kiongozi huyo wa Chama kuwa na jopo lake ambalo linashiriki kuuza maeneo na kuchochea migogoro katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi amewataka wakazi wa Bagamoyo kuacha kuvamia maeneo ya Serikali ambayo hayajaendelezwa likiwemo la Lazaba linalomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amehaidi kufanyia kazi maelekezo ya Waziri kukomesha uvamizi wa Mkoa huo, huku akieleza migogoro mingi katika Wilaya hiyo inadaiwa kuchangiwa na watendaji na Viongozi wa kisiasa.