Watu watano wanashikiliwa na polisi mkoani Tabora kwa tuhuma za mauaji ya askari wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ), Samweli Anton (28) wa kikosi 262 Milambo, aliyeuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Mkuu wa wilaya ya Tabora mjini, Komanya Kitwal amesema watu hao wamekamatwa kutokana na msako wa polisi huku majina ya waliyokamatwa yakihifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi.
Akielezea jinsi alivyouawa amesema ” Alikutwa na mauti baada ya kuachana na wenzake aliokuwa nao kwenye doria ya ulinzi shirikishi wa mtaani kwake, wakati akiwa njiani kurejea nyumbani ndipo alikutana na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka, walimpiga kichwani na kumsababishia kifo”.
Aidha DC Komanya amewataka wananchi wanaomiliki silaha kuzisalimisha polisi kuanzia April 6 hadi Mei 4 na wale wanaomiliki kihalali wazipeleke kuhakikiwa kwani baada ya muda huo kupita watakaobainika watakamatwa na kufikishwa Mahakamani.