Washambuliaji Gareth Bale na Sergio Aguero wamekua miongoni mwa wachezaji watano waliotajwa kwenye orodha ya awali, iliyotolewa na uongozi wa French Football Magazine, ambao wanaratibu zoezi la utoaji wa tuzo ya Ballon d’Or.
Orodha ya wachezaji 30 inatarajiwa kutajwa kuanzia leo jumatatu, na tayari majina matano yameshatolewa kwa kigezo cha kufuata alfabeti.
Mshambuliaji Bale ameungana na mwezake wa Real Madrid Karim Benzema pamoja na Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain.
Mlinda mlango wa majogoo wa jiji Liverpool Allison, naye ametajwa kwenye orodha ya awali, ambayo inaacha nafasi ya wachezaji wengine 25 kutajwa baadae.
Kwa mujibu wa utaratibu wa alfabeti, inadhihirisha mshambuliaji wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang na mlinda mlango wa PSG Gianluigi Buffon hawana nafasi ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Hata hivyo orodha inayotarajiwa kutolewa baadae, inategemewa kuwa na majina mazito ya wachezaji kama Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Luka Modric, Kylian Mbappé na Neymar.
Kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Croatia Luca Modric, bado anapewa nafasi kubwa ya kuendelea kutamba katika tuzo msimu huu, baada ya kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya na FIFA.
Ronaldo na Messi wamekua wakitawala katika tuzo za dunia tangu mwaka 2008, ambapo kila mmoja ameshatwaa tuzo tano, lakini kwa mwaka huu Modric ameonyesha kuzima mfumo huo, na kinachosubiriwa ni kwa upande wa Ballon d’or kama ataweza kuwabwaga manguli hao.
Orodha ya awali ya wachezaji watano iliyotolewa.
- Allison (Liverpool)
- Sergio Aguero (Manchester City)
- Gareth Bale (Real Madrid)
- Karin Benzema (Real Madrid)
- Edinson Cavani (Paris Saint-Germain)