Jumla ya watu 19,681 ,259 wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kushiriki zoezi la uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa nchini Novemba 24, 2019 ambapo kati ya hao wanaume 9,529,992 na wanawake 10,151,267 sawa na asilimia 86 ya lengo la uandikishaji wa wapiga kura 22,916,412.
Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo ameyasema hayo Jijini Dodoma na kudai kuwa uandikishaji wa mwaka huu una mafanikio ikilinganisha na uchaguzi wa mwaka 2014 kwani serikali ilikadiria kuandikisha watu 18,787,820 na waliojiandikisha ni 11,882,086 sawa na asilimia 63% ya makadirio.
“Haya mafanikio ya mwaka huu wa 2019 katika uandikishaji wa wapiga kura yametokana na hamasa kubwa iliyofanywa na Viongozi wa Kitaifa, Viongozi wa ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ngazi ya Makao Makuu, Wizara hadi ngazi za chini za vitongoji, vijiji, wananchi na vyombo vya habari,” ameongeza Jafo.
Ameitaja Mikoa mitano iliyoongoza katika uandikishaji kuwa ni Dar es salaam iliyotaraji kuandikisha watu 2,673,873 huku uandikishaji halisi ukiwa ni watu 2,898,535 sawa na asilimia 108, Pwani lengo la watu 594,247 na kupata watu 568,627 sawa na asilimia 96, Mwanza lengo watu 1,404,078 na idadi halisi ikiwa ni watu 1,340,177 sawa na asilimia 95.
-
Video: MAJONZI! kijana aliyepumlia Mashine, alikisema kifo chake, Neno lake la mwisho lawaliza ndugu
Mikoa mingine ni Tanga iliyotaraji kuandikisha watu 1,087,921 na kuvuka lengo kwa kupata watu 983,104 sawa na asilimia 90 na Mkoa wa Singida uliokuwa na lengo la kuandikisha watu 679,427 na kupata watu zaidi waliojiandikisha 610,344 ambao ni sawa na asilimia 90.
“Zipo pia Halmashauri tano zimefanya vizuri ya kwanza ni Halmashauri ya Mlele DC Malengo ni watu 17,848 na uandikishaji ukawa ni watu 27,196 sawa na asilimia 152, Ngorongoro DC malengo yalikuwa watu 75,145 na uandikishaji ni watu 96,622 sawa na asilimia 129,” amesema Waziri Jafo.
Nyingine ni Halmashauri ya Kibiti DC iliyokuwa na malengo ya watu 47,887 ns uandikishaji ukawa watu 60,539 sawa na asilimia 126, Halmashauri ya Temeke MC malengo watu 718,883 uandikishaji watu 879 ,619 sawa na asilimia 122 na tano ni Monduli DC Malengo ni watu 75,173 na uandikishaji ni watu 91,363 sawa na asilimia 122.
Aidha Jafo ameongeza kuwa uandikishaji wa wapiga kura ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya mvua kwa baadhi ya maeneo nchini pia wananchi wachache kuchanganya zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalofanywa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) na lile la uandikishaji wa daftari la orodha ya wapiga kura sambamba na umbali wa baadhi ya maeneo yaliyokuwa na vituo vya kujiandikisha.
Zoezi la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura lilianza rasmi Oktoba 8, 2019 na kumalizika Oktoba 17, 2019 huku uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa ukitarajia kufanyika Novemba 24, 2019.