Waamuzi Elly Sasi, Salim Mkono, Seif Mpanga na Martine Saanya wametajwa kuwa waamuzi wa Mchezo wa awali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya URA (Uganda) dhidi ya Ethiopian Coffee SC (Ethiopia).
Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la soka nchini TFF imeeleza kuwa waamuzi hao watachezesha mchezo huo utakochezwa katika uwanja wa St. Marry, mjini Kampala Septemba 12, 2021.
Kundi hilo la waamuzi kutoka Tanzania linakua la pili kutajwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF baada ya waamuzi wanne wengine kupangwa kuchezesha mchezo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baina ya Mogadishu City ya Somalia na APR ya Rwanda utakaochezwa Septemba 12 huko Djibouti.
Ramadhan Kayoko ndiye atakuwa mwamuzi wa kati ambapo atasaidiwa na Frank Komba na Soud Lila huku refa wa akiba akiwa ni Mfaume Ali Nassoro.
Katika hatua nyingine Watanzania wawili wameteuliwa kuwa maofisa wa mechi mbili tofauti za mashindano hayo.
Msafiri Mgoyi amepangwa kuwa kamishna wa mechi kati ya Zesco United ya Zambia na Royal Leopards ya Eswatini, Septemba 18 wakati Hamid Al-Busaidy atakuwa ofisa wa vipimo vya Uviko-19 katika mchezo baina ya KMKM na Al Ittihad utakaochezwa Septemba 19 kwenye Uwanja wa Amaan huko Zanzibar.