Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Manchali Kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, wametoa wito kwa Watanzania hasa wa Vijijini, kutumia vyema akiba ya chakula waliyonayo, ikiwemo kuwa waangalifu na matumizi yasiyokuwa ya lazima, kitu kitakachowasaidia kumudu mtikisiko wa maisha unaotokana na uwepo wa mambo mbalimbali ikiwemo janga la mabadiliko ya tabianchi.
Wakizungumza na Dar24 hivi karibuni, Wananchi hao wamesema kwa akili ya kawaida si vyema kuisubiri Serikali itoe tahadhari ya kila kitu, kwa kuwa kila mtu anajionea jinsi hali ya mabadiliko kimazingira na hali ya hewa Duniani, kutokana na taarifa mbalimbali za malalamiko ya maafa zinazotangazwa na vyombo vya Habari kila kukicha.
Mmoja wa Wakazi wa eneo hilo, Robert Magayo amesema, “Tazama jua lilivyo kali, zamani mida kama hii tayari mvua zinaunguruma watu wanaandaa mashamba kwa ratiba za kichwani za kukariri lakini kwasasa hakuna uhakika, tunasikia nchi nyingine zina mafuriko, ukitazama kwetu ni jangwa sasa hii ni ishara ya kuwa waangalifu na bila chakula unakufa, tutunze chakula jamani.”
Naye mkulima wa siku nyingi, Chiko Barabara amesema pamoja na tishio hilo lakini ni vyema maisha ya kawaida yakaendelea na kwamba watu waendelee kuchukua tahadhari huku wakifurahia maisha na kusisitiza juu ya suala la amani kwakua ndiyo msingi wa Taifa, wakati wakitafuta mbinu mbadala za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kwa ushirikiano na Serikali.