Uongozi wa Azam FC umefichua mipango ya usajili kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa kwa kuahidi kusajili wachezaji watatu pekee.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Amin ‘Popat’ ameeleza kuwa wanafanya hivyo kutokana na ubora na upana wa kikosi chao msimu huu licha ya kushindwa kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
“Tutaongeza wachezaji watatu kati ya hao wawili tumeshamalizana nao kila kitu tunasubiri ligi imalizike ili tuwatambulishe lakini mmoja ndio tunaendelea naye na mazungumzo naamini baada ya wiki mbili kila kitu kitakuwa tayari,” amesema Popat.
Kiongozi huyo amesema malengo yao kwa msimu unaokuja wa 2023/24 ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu lakini pia kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho wanayotarajia kushiriki kutokana na nafasi waliyopo kwenye ligi na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Popat amesema anajua vita hiyo siyo ndogo lakini msimu ujao wamejipanga kupambana na fitna pamoja na changamoto zote ili kuhakikisha wanabeba ubingwa wa Tanzania Bara.
Azam FC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23 ikiwa na alama 53 lakini pia imetinga Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na watacheza Fainali na mshindi kati ya Singida Big Stars na Young Africans.