Imefahamika kuwa jumla ya wachezaji watatu tegemeo wa Power Dynamos ya nchini Zambia, wanatarajiwa kuukosa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba SC.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumapili (Oktoba Mosi) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam baada ya mchezo wa kwanza ugenini kutoka sare ya mabao 2-2.

Taarifa kutoka Zambia zinaeleza kuwa, Power Dynamos itawakosa wachezaji wake muhimu katika kikosi cha kwanza kutokana na majeraha.

Wachezaji hao wawili watakosekana kutokana na majeraha waliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu ya Zambia waliocheza mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Zesco United.

Jarida hilo liliwataja wachezaji hao ni, Mlinda Lango chaguo la kwanza Lawrence Mulenga na beki Aron Katebe ambao wote wanauguza majeraha.

Mwingine ni beki Dominic Chanda ambaye yeye anaitumikia adhabu ya kadi nyekundu.

“Power Dynamos FC imethibitisha rasmi kwamba kuelekea katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Simba SC, itakosa huduma kutoka kwa baadhi ya wachezaji wao muhimu wa kikosi cha kwanza kutokana na majeraha na adhabu ya kadi nyekundu.

“Wachezaji hao ni kipa Lawrence Mulenga aliyeumia katika mchezo dhidi ya Zesco United, beki Dominick Chanda ambaye ana majeraha,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezungumzia hilo kwa kusema: “Hivi sasa hatuwaangalii wapinzani wetu nini wanafanya, badala yake tunaelekeza nguvu zetu katika maandalizi ya kikosi chetu.

“Sisi katika mchezo huo, tutawakosa baadhi ya wachezaji wetu kama Kramo (Aubin), Manula (Aishi) na Inonga (Hennock) wenye majeraha.”

Mashabiki Power Dynamos waifuata timu yao Dar
Mgao wa umeme kuendelea hadi Machi 2024