Wachezaji Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho na Mzamiru Yassin wamerejea katika shughuli zao, baada ya kupona majeraha yaliyowafanya kukosa michezo kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Wachezaji hao watatu walikua miongoni mwa wachezaji watano wa klabu ya Simba waliokua wanasumbuliwa na majeraha, hali iliyosababisha benchi la ufundi kuwaweka pembeni na kuwatumia wachezaji wengine.
Chumba cha majeruhi cha Simba, kilikuwa na wachezaji watano muhimu wa kikosi cha kwanza, lakini sasa wamebaki wawili baada ya klabu hiyo kutangaza kurejea mazoezini kwa viungo.
“Sadio Kanoute, Pape Ousmane Sakho na Mzamiru Yassin, wamepona majeraha yao na wamerudi uwanjani wakiwa fiti kwa asilimia 100,” ilieleza taarifa hiyo ya Simba.
Tayari Kanoute na Sakho wameanza mazoezi pamoja na wenzao tangu mwanzoni mwa juma hili wakati Mzamiru amejiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachojiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya DR Congo, mchezo ambao utakaopigwa kesho Alhamis (Novemba 11) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Wachezaji wengine waliokuwa majeruhi, Kiungo Taddeo Lwangwa, uongozi wa Simba ulieleza yeye bado anauguza jeraha na amepewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kurejea uwanjani kuuwahi mchezo dhidi ya Ruvu Shooting utakakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Novemba 19, mwaka huu.
Kuhusu mshambuliaji Chris Mugalu, “yeye ataendelea kukosekana kwa sababu ya jeraha linalomsumbua kutopona vizuri, hivyo amepewa muda ili awe fiti kwa asilimia 100”.