Watawa wawili wa kiume wa kanisa la Khufti (coptic), wamehukumiwa kifo nchini Misri kwa mauaji ya askofu mwaka 2018, maafisa wa Cairo wamethibitisha.
Askofu Epiphanius (64), alipatikana ikiwa ameuawa na kuvuja damu nyingi ndani ya makazi ya kanisa kaskazini mwa jiji la Cairo mwezi Julai 2018.
Mamlaka za Misri zilihusisha tukio hilo na ugomvi ambao haujawekwa wazi baina ya watawa hao na Askofu, huku hukumu ya kunyongwa ilipitishwa mwezi Februari mwaka huu na kisha kupelekwa kwa mufti mkuu wa Misri ili kupitiswa.
Jumatano wiki hii Mahakama ya Damanhur ilithibitisha kuwa kutokana na ushahidi uliopatika katika kesi hiyo na maridhio ya Mufti, hukumu ya kifo juu ya watawa hao imepitishwa.
Mmoja wa watawa hao, Wael Saad, ameripotiwa kukiri mbele ya waendesha mashtaka kuwa alitumia nondo kumshambulia askofu huyo mpaka kufikwa na umauti, mtawa mwingine Remon Rasmi, alishtakiwa kwa kosa la kumpatia Saad usaidizi.
Watawa hao Saad na Rasmi ambao pia walikuwa wakifahamika kwa majina yao ya kikanisa kama Ashiah, Faltaous, wanaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Kesi hiyo imewaacha wengi ndani ya kanisa la Khufti na bumbuwazi na baada ya tukio hilo kiongozi wao Papa Tawadros II, ametangaza kusitisha uandikishaji wa watawa wapya kwa kipindi cha mwaka mzima, na watawa wote watatakiwa kufunga kurasa zao za mitandao ya kijamii.
Wakhufti walijitenga na madhehebu mengine ya kikristo mwaka 451, hivyo ni moja ya makanisa makongwe zaidi duniani na kanisa hilo linachukuliwa kuwa ndio kubwa zaidi katika mashariki ya kati na lina wafuasi milioni moja nje ya Misri.