Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaagiza Viongozi na Watendaji Mkoani humo kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo bora na kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya kaya ambazo hazina vyoo, ili kukabiliana na ugonjwa wa mlipuko wa kuharisha na kutapika.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi cha Mkoa kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo hivi karibuni, Serukamba amesema maradhi hayo husababishwa na mazingira ya uchafu hivyo jamii inapaswa kuhakikisha mazingira yote yanayowazunguka yanakuwa safi kwa lengo la kudhibiti magonjwa ya mlipuko hasa Kipindupindu ili kisiwepo kabisa Mkoani Singida.
Aidha, Serukamba amewasisitiza Wakuu wa Wilaya wote Mkoani humo kuhakikisha maeneo yote ya kaya, taasisi za umma, mashirika ya dini, masoko, stendi za mabasi, mashuleni, kwenye nyumba za ibada na mikusanyiko rasmi na isio rasmi kuwa na vifaa vya kunawia mikono, maji safi na sabuni ili kujikinga na maradhi hayo.
Amewasisitiza Wakuu hao wa Wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo yote ya kupikia na kuuzia vyakula yanakaguliwa na wataalamu wa Afya ili kuwa safi muda wote. Aidha kila Halmashauri ifanye kikao cha kamati ya Afya ya Msingi pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.