Watendaji wa mamlaka za maji nchini wametakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wazidishe juhudi na kutumia ubunifu walionao ili kukuza mapato ya sekta hiyo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo mjini Singida katika ufunguzi wa mkutano wa uendeshaji wa kisekta baina ya wakurugenzi wa mamlaka za maji na watendaji wakuu wa sekta hiyo.
”Mamlaka za maji zinaendelea kutoa huduma lakini ubunifu ni suala lililo kando hivyo ubunifu unahitajika ili kuleta maendeleo ya kisekta na pia ujenzi wa miradi ya maji ni mabadiliko chanya hivyo zingatieni suala hili,” ameongeza Prof. Mkumbo.
Amesema kutokana na mabadiliko hayo ipo haja ya kupitia muundo mpya wa utumishi kuanzia ngazi ya Wizara na taasisi ili kuiweka katika mifumo inayoeleweka na hatimaye kufikia malengo kusudiwa yatakayoleta mabadiliko nchini.
Aidha Prof. Mkumbo amebainisha kuwa kupitia mfumo huo mpya itasaidia taasisi husika kuweza kuchagua wahandisi wenye viwango stahiki kukidhi matarajio ya miradi kwa ufanisi na kuifanya sekta hiyo kuwa na miundombinu bora na ya kudumu.
“Tunakusudia kuanza kuzingatia vigezo ikiwemo kuangalia ni mradi gani apewe mkandarasi kulingana na sifa na uwezo alionao kuweza kusimamia mradi husika hii itasaidia kuondoa na kuzuia upotevu wa pesa za serikali na kupata miundombinu imara,” amebainisha Katibu huyo.
Hata hivyo Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa suala hilo litafanikiwa endapo kutakuwepo na ushirikiano wa dhati baina wa watendaji wa sekta ya maji, wadau na jamii nzima nchini katika maeneo yenye miradi husika.