Jumla ya watoto 36 wenye umri wa chini ya miaka nane wamefanyiwa vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 Wilayani Ikungi Mkoani Singida.
Hatua hiyo imepelekea Wilaya kuweka kusudi la kutumia zaidi ya shilingi milioni 110 mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalum cha kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa programu jumuishi ya Taifa inatakayoendelea hadi mwaka 2026 inayohusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto .
“Kati ya kesi hizo 36, tisa zipo mahakamani, moja ilifungwa na kituo cha polisi, nyingine iko katika rufaa Ustawi wa Jamii na zilizobaki watuhumiwa hawakuweza kupatikana,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Amesema watoto hao walifanyiwa ukatili wa kingono, kimwili, kihisia na imewafanya kupata madhara ya kisaikolojia, magonjwa, ulemavu, kupoteza ndoto zao, haki ya elimu na kuleta ongezeko la watoto waishiomazingira magumu.
Muro ameongeza kuwa, pamoja na mradi huo kuwepo kwenye utekelezaji wa programu
Jumuishi ya Taifa, mradi huo umetokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayoelekeza kila wilaya kukomesha matukio na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Mradi huu mkubwa wa aina yake umetokana na maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayoelekeza kila wilaya kukomesha matukio na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake chini ya ufadhili wa hirika lisilo la kiserikali la KIWOHEDE,” amesema.
Ujenzi huo unatarajia kuendana na utoaj wa elimu mashuleni juu ya upingaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuanzisha kamati za ulinzi wa mwanamke na mtoto kwa kushirikisha jamii, wadau na Jeshi la Polisi.