Waasi wa Allied Democratic Forces – ADF, nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC wanadaiwa kuwavisha mikanda yenye vilipuzi mapacha wawili wa kike wenye umri wa mwaka mmoja, ikiwa ni mtego kwa vikosi vya usalama, kitendo ambacho kimetafsiriwa kuwa ni ukatili kwa watoto.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Watoto hao wa kike waligundulika katika kijiji kimoja kilichopo Kivu Kaskazini, eneo ambalo kundi la Wanamgambo hao limezidisha mashambulizi ya mabomu, hatua ambayo imelaaniwa na Shirika linaloshughulikia watoto la UNICEF.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Congo, Grant Leaity amesema Vilipuzi hivyo vilifanikiwa kuondolewa na wataalamu wa kutegua milipuko huku ikidaiwa kuwa vilitegwa kuwalenga Polisi au Wanajeshi wa Congo walipowasili na kuchochea mlipuko dhidi ya majeshi ya usalama.
Mapacha hao, hata hivyo bado hawajatambuliwa na wanapatiwa huduma katika kituo cha Umoja wa Mataifa kabla ya kupelekwa katika kituo cha malezi na inadaiwa kuwa Wazazi wao wameuawa katika shambulio linaloaminika kutekelezwa na ADF na afya zao zinaendelea vizuri.
Wakatai huohuo Msimamizi wa eneo la Irumu, Kanali Jean Siro Simba Bunga kulikotokea tukio hilo amesema watu wasiojulikana wakiwa na Silaha wamekishambulia kijiji kimoja katika jimbo la Ituri mashariki mwa Congo na kuua takriban watu 18 na kujeruhi 12, huku wakichoma miili mitatu na kuzika mingine 15.