Serikali imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Majiji kuwakamata watoto wanaombaomba mitaani ili washtakiwe kwa mujibu wa sheria inayokataza utoro shuleni.
Agizo hilo limetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda ambaye amesema ombaomba bado ni tatizo katika jiji la Dar es Salaam.
“Mfano Septemba 2013, ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa kwao, ambapo watoto 32 walirejeshwa shuleni na hii inathibitisha kuwa wapo watu wazima wanaowatumia kuomba, nawaagiza wakurugenzi kuwakamata watoto wote wanao ombaomba mitaani ili washtakiwe kwa mujibu wa sheria inayokataza utoro mashuleni,” alisema Kakunda.
Kakunda alikuwa akijibu swali la Ibrahim Raza Mbunge wa Kiembe Samaki, ambaye alihoji ni lini serikali itachukua hatua kuwaondoa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema mara nyingi ofisi ya mkuu wa mkoa imekuwa ikichukua hatua za kuondokana na tatizo hilo kwa kuwarudisha makwao.