Uchumi wa Mataifa Mengi barani Afrika umekuwa ukishikiliwa na watoto wa Wakulima na Wafugaji, na hivyo kufanya uwepo wa hitaji la mafunzo kwa jamii hizo ili waweze kujiendesha kisomi na kuimarisha uchumi wa pato lao na Taifa kiujumla.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Kahama, Jumanne Kishimba wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media na kuongeza kuwa, karibu asilimia 90 ya vitu vinavyotumiwa na mataifa mengi ikiwemo Tanzania vimekuwa vikitengenezwa au kuzalishwa na jamii hiyo.
Amesema, “na jamii ya watu hawa ndio walioshikilia uchumi wa Tanzania ndio wanaoamka saa kumi kwenda kulima, ndio wanaochunga na asilimia 90 ya vitu tunavyotumia nchini wanatengeneza wao na ule mpango wa Tableti ungewahusu ili wakati wanaendelea kuchunga wanakuwa wanajisomea pia.”
Aidha, Kishimba ametolea mfano kuwa katika jimbo lake wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiuliza Korona itarudi lini kwani wanawaza faida kutokana na shule kufungwa katika kipindi hiko ambapo walitengeneza faida kubwa baada ya kutumia muda hu kulima na kupata mazao maradufu.