Watoto wa Tanzania, wameipongeza Serikali kwa juhudi inazozionesha za kuhakikisha kuwa wanapata Elimu, huduma za kiafya na kuweka mifumo mbalimbali ya ushirikishwaji wao ikiwemo mabaraza ya watoto huku wakitaka hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya ndoa za utotoni kwani sheria ya mwaka 1971 bado inaruhusu mtoto wa kike chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.
Wakizungumza hii leo Novemba 19, 2022 katika mkutano wao na waandishi wa Habari kuzungumzia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Watoto itakayofanyika hapo kesho Novemba 20, 2022, wamesema licha ya Tanzania kusaini mikataba ya kimataifa ya kulinda haki za watoto lakini michakato imekuwa mingi huku watoto wa kike wakiendele kuumia.
Aidha, kupitia taarifa yao wameeleza kuwa, “Muongozo wa Serikali wa kuhakikisha watoto wanaoacha shule hasa wale wanaopata ujauzito wanarudi shuleni umetolewa, japo utekelezaji wake unasuasua na tunahimiza wadau kutoa elimu juu ya muongozo huu ili watoto waweze kusaidiwa kurudi shuleni.”
Hata hivyo, watoto hao wamesema wana haki ya kushirikishwa katika mambo yanayohusu makuzi yao, na kuwashukuru wazi na walezi ambao wamekuwa wakiendelea kuwalea, kuwahudumia na kuahidi kutimiza wajibu wao wa kitanzania kwa kuzingatia maadili na utamaduni huku wakiomba kupatiwa muda wa kupumzika, kucheza na kuungana na marafiki.