Wamiliki wa Nyumba za kulala wageni, wametakiwa kutowapokea watoto chini ya umri wa miaka 18 au wanafunzi pindi wanapokuja na wenza wao katika nyumba za kulala wageni kwa lengo la kufanya anasa, badala yake watolewe taarifa, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi wa Polisi Sidney Elias alipokuwa akitoa elimu kwa wafanyabiashara na wamiliki wa nyumba za kulala wageni nje ya kituo cha Polisi Lupiro Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa lengo la kuisaidia Polisi kuzuia uhalifu.
Amesema, wamiliki hao pia wanatakiwa kuongea na wahudumu ili waweze kujenga tabia ya kutoa taarifa za wageni wahalifu, pindi wanapowatilia mashaka lakini pia wahakikishe kila mgeni anajaza taarifa zake kwenye kitabu.
Wakati huohuo, Wafanyabiashara wa Kata ya Kidodi Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wametakiwa kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wananchi wanaounda Vikundi vya Ulinzi Shirikishi, ambavyo vimekuwa msaada mkubwa katika kuzuia matukio ya uhalifu.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Aiden Mufundi wakati akitoa elimu kwa Wafanyabiashara mbalimbali katika Kata ya Kidodi iliyopo Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Amewataka pia wafanyabiashara hao kuweka taa zenye mwanga mkali kwaajili ya ulinzi na wale wenye biashara kubwa zaidi waweke CCTV kamera ili ziwasaidie kuzuia wahalifu na kuwatambua kwa haraka endapo wizi utatokea.