Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka watoto kote nchini kufichua viashiria vya vitendo vya ukatili dhidi yao vinavyotokea katika maeneo ya shule na nyumbani.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma hii leo Juni 6, 2022, wakati akiongea na Wanafunzi, Walimu na Waandishi wa Habari katika Shule ya Msingi Mnadani iliyopo jijini Dodoma ikiwa ni chache kabla ya kilele cha siku ya Mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa Juni 16 ya kila mwaka.
”Wanangu Baba akikukatli mwambie Mama na kama ni Mama basi mwambie Baba, au kama unaona huwezi kumwambia Baba au Mama basi mwambie mtu unayemwamini,” amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima pia amewasisitiza watoto hao kutokuogopa waonapo vitendo vya ukatili au viashiria na kuwataka watoe taarifa kwa watu wanao waamini ikiwepo dawati la jinsia linalopatikana kwenye vituo vya Polisi nchini.
Akitoa hali ya takwimu ya matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021, Gwajima amesema jumla ya matukio yaliyoripotiwa ndani ya Jeshi la Polisi ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, sawa na upungufu wa imatukio 4,371 sawa na asilimia 27.5
“Mikoa iliyoongoza ilikuwa ni Arusha 808, Tanga 691, Shinyanga 505, Mwanza 500 na Mkoa wa Kipolisi Ilala 489. Akisema makosa yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji 5,899, mimba kwa wanafunzi 1,677 na ulawiti 1,114,” amefafanua Dkt. Gwajima.
Aidha amesema msingi wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika ni utoaji wa haki za Mtoto kama ilivyoelekezwa na Umoja wa Afrika katika mkataba wa haki na ustawi wake wa mwaka 1991 . “Umoja wa Afrika ulitohoa maazimio hayo kutoka katika Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa mwaka 1989,” amefafanua Dkt. Gwajima.
Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa Mwaka 2022 ni “Tuimarishe ulinzi wa Mtoto; Tokomeza Ukatili Dhidi Yake: Jiandae kuhesabiwa” ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na hatimaye kuvitokomeza kabisa.
Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na Watoto iliandaa sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha haki tano za msingi za Mtoto ikiwepo ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki, kutobaguliwa na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009.