Watu 18 wameuawa kufuatia mapigano mapya yaliyozuka kati ya koo mbili usiku wa kuamkia Jumamosi, katika jimbo la Warrap lililopo Kaskazini mwa Sudan Kusini.
Kamishna wa eneo hilo Samuel Awan, amesema watu 34 walijeruhiwa kwenye mapigano hayo wakati ambapo uhasama unaongezeka kwenye maeneo ya vijijini nchini humo.
Mapigano hayo kati ya koo mbili zinazopingana, yalisababishwa na kuuawa kwa mtu mmoja mnamo siku ya Alhamisi jioni ambapo kwa mujibu wa taarifa mtu huyo aliuawa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha jambo lililozusha lawama kati ya pande hizo mbili hasimu.
Maafisa wanahofia kuzuka tena kwa mapigano zaidi iwapo serikali haitaingilia kati kwa haraka.
Mnamo mwezi Agosti zaidi ya watu 100 waliuawa katika mkoa huo wa Warrap pale raia walipopambana na jeshi kuhusu zoezi la upokonyaji silaha baada ya askari wa Sudan Kusini wa kikosi cha Ulinzi wa Watu, walipojaribu kuwapokonya silaha raia katika mji wa Tonj Mashariki mwa nchi hiyo kama sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa hivi karibuni.