Serikali ya Zimbabwe imewafuta kazi wauguzi zaidi ya 10,000 waliokuwa kwenye mgomo Jumatatu wakishinikiza kuongezwa mishahara na kuboreshewa mazingira ya kazi.
Makamu wa Rais, Constantino Chiwenga amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya wauguzi hao kukataa kurejea kazini baada ya kutengewa $17milioni kwa ajili ya ongezeko la mishahara yao kwa ujumla.
Chiwenga alilaani mgomo wa wauguzi hao akieleza kuwa wametelekeza maisha ya wananchi wa taifa hilo.
“Serikali imeamua kwa maslahi ya wagonjwa wa taifa hili na kuokoa maisha, tumeamua kuwafuta kazi wauguzi wote waliogoma, kuanzia sasa, “ alisema Jenerali Chiwenga.
Rais Emmerson Mnangagwa aliahidi kuboresha sekta ya afya kama moja kati ya vipaumbele vikuu vya serikali yake. Aliahidi kuongeza mishahara ya wauguzi na madaktari nchini humo katika hatua ya kuwapa motisha ya kufanya kazi ya kuwahudumia vizuri wagonjwa.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanadai kuwa hiyo inaweza kuwa ni hatua ya kuwalazimisha warejee kazini kuhofia kupoteza kabisa nafasi zao, endapo Serikali itatangaza kuwapa nafasi nyingine.
Chama cha wauguzi kimedai kuwa kimeipokea taarifa hiyo ya Serikali, lakini bado kinaendelea na mgomo wake kama kawaida kwa wauguzi wote.