Watu wenye silaha wamevamia kanisa wakati wa ibada na kuua watu 16 ikiwa ni pamoja na mchungaji aliyekuwa akiongoza ibada katika mji mkuu wa Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Tukio hilo limetokea mapema wiki iliyopita katika kanisa la Notre-Dame de Fatima church. Washambuliaji hao wanadaiwa kuwa walikuwa wamejihami pia na vilipuzi na maguruneti.
Mashambulizi ya nyumba za ibada yamekuwa yakiripotiwa nchini humo kutokana na kuendelea kuwepo mgogoro wa kidini na kikabila uliodumu kwa miaka kadhaa.
Wiki iliyopita, mashambulizi mengine yalifanyika katika eneo la msikiti mkubwa jijini humo na kusababisha vifo vya watu 23.
Ingawa vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa watu 15 ndio waliofariki, Redio ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI) imekariri ripoti ya Msalaba Mwekundu ikieleza kuwa watu 16 walifariki na wengine 99 walijeruhiwa.
Kutokana na tukio hilo, umati wenye hasira waliubeba mwili wa mchungaji aliyeuawa na kuupeleka karibu na eneo la Ikulu ya nchi hiyo. Wanaishutumu Serikali kwa kushindwa kuwadhibiti waasi na kudumisha usalama.