Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said, amethibitisha Klabu hiyo kuingia Sokoni katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili, ili kukiongezea nguvu kikosi chao.
Young Africans ipo katika vita ya kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu, na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, huku ikiwa miongoni mwa Klabu 16 zilizotinga Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumanne (Desemba 20), Kiongozi huyo amesema kwa mujibu wa ripoti ya Benchi lao la Ufundi, wanalazimika kuingia sokoni kusaka wachezaji wawili wa Kimataifa, ambao watakuwa na ubora wa hali ya juu.
Amesema kama ilivyo kawaida ya Klabu hiyo, Mchezaji atakayeajiliwa anapaswa kuwa na uwezo wa hali ya juu dhidi ya waliopo kikosini hivi sasa, hivyo watahakikisha wanafuata sera hiyo ili kuwa na kikosi imara.
“Huu ni wakati wetu Young Africans SC kuweka alama kwenye mashindano ya kimataifa. Na sisi Wanayanga mfumo wetu ni ule ule mchezaji tunayemsajili lazima awe bora sana au zaidi ya yule ambaye tunaye” amesema Injinia Hersi Said
Hadi sasa Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 41, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 37 huku Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 36.
Kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara Young Africans imetinga hatu ya 32 Bora baada ya kuichapa Kurugenzi FC ya Simiyu mabao 8-0.
Katika upande wa Kimataifa Young Africans imepangwa Kundi D la Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika sanjari na Klabu za US Monastir (Tunisia), TP Mazembe (DR Congo) na Real Bamako (Mali).