Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo amemuagiza mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye kuwakamata na kuwekwa ndani viongozi na wasimamizi wa miradi wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) mkoani humo kwa kuchukua fedha za miradi na kushindwa kuitekeleza.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo akiwa wilayani Uvinza mkoani Kigoma wakati akikagua miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwemo nyumba ya mkuu wa Wilaya Uvinza, na za watumishi na hospitali ya wilaya hiyo.
“Nataka kuorodheshewa miradi yote iliyokwama kwa mkoa wa Kigoma ambayo ilikuwa inatekelezwa na TBA, nielezwe thamani ya kazi iliyofanyika na kiasi cha fedha kilichotolewa na taarifa hiyo iwasilishwe ofisini kwangu mara moja ili niweze kuifanyia kazi,” amesema Jafo.
Amesema amechukua uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kuwa TBA imepewa Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mkuu wa wilaya huyo miaka mitano iliyopita lakini hadi leo umejengwa msingi pekee.
Awali, akitoa taarifa kwa Jafo meneja wa miradi ya ujenzi Mkoa wa Kigoma, Masawika Kachenje amesema miradi hiyo ilianza mwaka 2013 na ilipaswa kukamilika 2018.
“Utekelezaji umekuwa mgumu kwa sababu fedha zimeenda TBA makao makuu na huku kwenye miradi fedha hazipelekwi na hivyo miradi umekwama, tumeshavunja mikataba yote na tumewaandikia barua tangu mwaka 2019 fedha zirudishwe lakini hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika,” amesema Machenje.