Mkuu wa Polisi nchini Ukraine, Ihor Klymenko amesema watu 16 akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine na maafisa wengine wakuu wa wizara wamepoteza maisha katika ajali ya helikopta iliyotokea nje ya Mji Mkuu wa Kyiv hii leo.
Taarifa ya Klymenko imesema kati ya watu hao waliopoteza maisha wawili ni watoto, 9 kati ya waliouawa walikuwa ndani ya helikopta ya huduma za dharura.
Amesema watu 22 wamejeruhiwa katika ajali hiyo wakiwemo watoto 10 huku taarifa zikieleza kuwa helikopta hiyo imeanguka karibu na jengo la shule ya watoto eneo la Brovary huko Kyiv.
Aidha Klymenko ameeleza kuwa waliopoteza maisha ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Denys Monastyrskyi, naibu wake Yevhen Yenin na Katibu wa Jimbo la Wizara ya Mambo ya Ndani, Yurii Lubkovych na wengine.
Hata hivyo hakuna taarifa za moja kwa moja zinazohusisha chanzo cha ajali hiyo,imeripotiwa kuwa uchunguzi utaanza mara moja kubaini chanzo cha ajali hiyo.