Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini wametakiwa kufuatilia upotevu wa shilingi bilioni 127 zilizoibwa katika vyama vya ushirika ambapo shilingi bilioni 2.5 kati ya hizo ni pesa za zao la ufuta pekee la sivyo Tume hiyo itavunjwa.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma Oktoba 25, 2019 na kudai kuwa Makamishna wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini wamekuwa hawatekelezi majukumu yao kikamilifu.
“Wizi wa mali na fedha za ushirika ni ishara ya makamishna kutofanya majukumu yao ipasavyo na jambo hili linapelekea Wanachama kuteseka na kukosa imani kutokana na ubadhirifu uliokithiri na hii inaonesha viongozi hawatekelezi wajibu wao,” amebainisha Waziri Hasunga.
Waziri Hasunga ambaye alikua kwenye kikao kazi cha Makamishna wa Tume amesema hakuna sababu ya kuwa na Tume ya Ushirika isiyotekeleza majukumu yake ipasavyo na kwamba serikali ina lengo zuri la ujenzi imara wa ushirika lakini wapo watu wasio na nia njema wanaoweka urasimu katika utendaji.
Kufuatia hatua hiyo Hasunga amemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya ushirika Dkt. Titus Kanani kuchukua hatua za haraka kwa watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao kikamilifu huku akisema endapo ushirika utasimamiwa vizuri wananchi watapata maendeleo na uchumi wa Taifa kukua.
Awali Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Titus Kamani amemshukuru Waziri wa Kilimo kwa kushiriki kikao hicho huku Kamishna wa Tume hiyo Mudhihir M. Mudhihir akimuhakikisha Hasunga kuwa Tume hiyo itatekeleza majukumu yake kwa weledi.