Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewahakikishia wadau wa habari kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari na kwamba Serikali ina nia ya dhati katika kufanikisha jambo hilo.
Nape, ameyasema hayo hii leo Novemba 21, 2022 jijini Dar es Salaam katika kikao chake na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), na kuongeza kuwa, Serikali imepokea maoni yao kuhusu marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya 2016.
Kikao hicho cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI), na serikali, cha kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, kiliongozwa na Nape mwenyewe ambaye amezini kufafanua kuwa, “Tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,.”
Mara baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema upo muelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari na kuongeza kuwa, ‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ya tangu mwanzo, tumemaliza na serikali inaendelea na hatua kabla ya kupelekwa bungeni.”
Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na kufutwa kwa mamlaka haya ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO), ili kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.
Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja na pia wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.
Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2)(b)(lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.
Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.
Sheria hizo, zinatajwa kuwa na vifungu vinavyofifisha uhuru wa habari nchini hivyo kuhitajika kubadilishwa ambapo kikao hicho kilishirikisha wadau na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama wa Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) na MISA- Tanzania.